Wednesday, 7 August 2013

Kenya kutoa mikopo isiyo na riba kwa biashara zinazoendeshwa na wanawake, vijana


Wafanyabiashara ya maziwa ya ngamia kutoka katika
 jamii ya Borana wakifungasha maziwa kwa ajili ya kutiwa
 katika majokofu huko Isiolo. Kuanzia mwezi Septemba,
 serikali itatoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake na
 vijana kuanza au kuboresha biashara zao. 
Serikali ya Kenya inapanga kutoa mikopo isiyo na riba
 ya shilingi bilioni 6
(dola milioni 68.7) mwezi Septemba kwa biashara zinazoendeshwa na vijana na wanawake.
Fedha hizo, zitakazojulikana kwa jina la "Mfuko wa Uwezo", mwanzo zilitengwa kwa ajili ya uwezekano wa kufanya duru ya pili ya uchaguzi wa rais baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Machi.
Wakati wa kuzinduliwa kwake tarehe 19 April, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kwamba serikali itaanzisha muundo wa kupanga tena malengo ya fedha hizo kufaidisha makundi hayo mawili ndani ya kipindi cha kwanza cha siku 100 ofisini, ambacho kiliisha tarehe 18 Julai.

"Tunatoa wito kwa vijana na wanawake wote kuwa tayari kwa mikopo hiyo," Makamu wa rais William Ruto alisema tarehe 28 Julai, akitangaza kutolewa mwezi Septemba. "Hatutawatoza riba yoyote hivyo wasiwe na uoga wa kuomba fedha hizo."

Mbunge wa Garissa Adan Duale alisema tarehe rasmi ya kutolewa itatangazwa Agosti, pamoja na wabunge wanawake wa kaunti na wabunge wa majimbo watakaofanya kazi kama wasimamizi wa pamoja wa mfuko huo.

Kamati za Mfuko wa Maendeleo ya Majimbo zitakuwa wasimamizi wa mfuko huo hadi kamati tofauti zitakapoundwa kwa ajili ya mfuko wa Uwezo, alisema.




"Kuchelewa kutolewa kwa fedha hizo kulitokana na uanzishaji wa muundo wa namna ya kutolewa fedha hizo," aliiambia Sabahi, akiongezea kwamba waombaji wanaweza kutuma maombi ya mikopo kupitia kwenye majimbo yao, ambayo yatapokea fedha hizo kutoka serikali kuu.

Vikundi vya vijana wapatao kumi wenye umri kati ya mika 18 hadi 36 lazima viwasilishe mpango wa biashara kustahili kukopa hadi shilingi 500,000 (dola 5,720), Duale alisema. Masharti kwa waombaji wanawake yatakuwa hayo hayo, lakini pasipo kikwazo cha umri.

Waombaji watatakiwa kulipa asilimia 3 ya kiasi cha mkopo katika ada za kushughulikia maombi, alisema.

"Kurejesha mkopo kutoka kwa mtu mmoja mmoja ni vigumu zaidi kuliko kurejesha kutoka kwa kikundi," alisema, akiongeza kwamba marejesho yatawezesha fedha kuwanufaisha watu wengi zaidi. "Mkopo lazima urejeshwe ili wale ambao hawakunufaika katika utoaji fedha wa kwanza waweze kunufaika katika utoaji unaofuatia."

Rachel Shebesh, mwakilishi mwanamke kutoka Kaunti ya Nairobi, alisema fedha zitasaidia kuongeza ukuaji wa uchumi kwa kuwawezesha wanawake na familia zao.

"Vijana na wanawake ni zaidi ya asilimia 60 ya idadi ya watu. Kwa kuwawezesha, Dira ya 2030 ya nchi itafanikishwa," aliiambia Sabahi, akiongeza kwamba Mfuko wa Uwezo utaongezea fedha zilizopo kama vile Mfuko wa Maendeleo ya Shughuli za Vijana na Mfuko wa Shughuli za Wanawake.

Justus Mochere, mwenye miaka 33, mweka hazina wa Kikundi cha Vijana cha Mwamanua katika Kaunti ya Kisii, alisema kikundi chake kimetuma maombi kwa Mfuko wa Uwezo ya shilingi 200,000 (dola 2,300) kupitia eneo la ubunge la Kitutu Chache.

Alisema Kikundi cha Vijana cha Mwamanua kinataka kuanzisha ufugaji wa kuku na kupanua mradi wa ufugaji wa samamki ambao unaendeshwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.

"Tumekuwa tukiepuka kuomba mikopo kutoka katika mifuko mingine kwa sababu ya kizuizi cha riba inayotozwa, lakini Mfuko wa Uwezo usio na riba ni mzuri kwetu," aliiambia Sabahi. "Tunatarajia kuuongeza na kusaidia familia zetu."

Mkaazi wa Garissa Abdikadir Hassan Abdi, mwenye miaka 29, alisema anatarajia fedha zitagawanywa kwa haki.

"Baadhi ya kamati ambazo zitasimamia Mfuko wa Uwezo awali zilikuwa na upendeleaji," alisema. "Kama kamati zitaendelea na mwelekeo wake wa upendeleo na ubaguzi, itakuwa njia ya kuleta wasiwasi kwa jamii, vita vya kikabila na kushindwa kwa mfuko huo."

0 comments:

Post a Comment