Shinikizo la kusitishwa Bunge la Katiba
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila
11.08.2014
Dar/Arusha. Joto la kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), linazidi kupanda nchini baada ya wabunge na vyama vya siasa kuendelea kusisitiza kuwa Bunge hilo halina tija kwa taifa.
Dar/Arusha. Joto la kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), linazidi kupanda nchini baada ya wabunge na vyama vya siasa kuendelea kusisitiza kuwa Bunge hilo halina tija kwa taifa.
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji
Christopher Mtikila amesema ameanza kukusanya saini za Watanzania
wanaopinga kuendelea kwa Bunge hilo ili kufungua kesi Mahakama Kuu ya
Tanzania, kusitisha vikao vinavyoendelea mjini Dodoma.
Mchungaji Mtikila akizungumza na Mwananchi
Jumapili alisema mchakato wa kukusanya saini hizo unaendelea katika
mikoa ya Arusha, Mwanza, Geita, Kagera, Dar es Salaam huku akibainisha
kwamba mwitio wa watu ni mzuri.
“Natafuta saini 20,000 za Watanzania na sasa
tayari tumekusanya saini zaidi ya 10,000 katika mikoa kadhaa na
natarajia Watanzania wataendelea kuniunga mkono ili kuhakikisha mchakato
huu. Nakwenda kuuzuia Mahakama Kuu na ninajua tu nitashinda,” alisema
Mchungaji Mtikila.
Alisema anakusanya saini hizo ili kudhihirisha
kuwa Watanganyika hawataki muungano, kwani mwaka jana Wazanzibari
walikusanya maoni 1,946 ya kupinga muungano.
Dk Chegeni
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Dk
Raphael Chegeni alisema kuendelea kwa Bunge hilo bila kuwepo kwa Ukawa
ni kuchezea fedha za umma.
Dk Chegeni alisema hayo jijini Arusha alipokuwa
akihudhuria vikao vya Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF), kwamba kuendelea na Bunge hilo ni kucheza kamari ya hatari
ambayo baadaye inaweza kusababisha malalamiko kwa wananchi na kuwagawa
wananchi.
“Sioni sababu ya haraka, huwezi kuandika katiba
bila ya maridhiano, haya mambo yenye utata itabidi yapatiwe muda mwafaka
na mchakato huu kuendelea baada ya uchaguzi mkuu mwakani.”
Dk Chegeni alisema, kwa kuwa kuna mahitaji ya
haraka yanayopaswa kuingizwa katika Katiba, ni busara Bunge la Novemba
kutumika kufanya mabadiliko hayo, ambayo ni pamoja na kuwa na Tume Huru
ya Uchaguzi, kuruhusu mgombea binafsi na pia kuingiza masuala ya haki za
binadamu kwenye Katiba.
Alisema hadhani kama kuna haraka sana wa kuandika
katiba wakati kuna kutoelewana, kwani Katiba inaweza kuandikwa hata na
utawala ujao, ingawa nia nzuri ya Rais Jakaya Kikwete ilikuwa ni
kuwaachia Watanzania Katiba Mpya.
Akizungumzia malumbano juu ya watu wanaotoa maoni
ya mchakato wa Katiba nje ya Bunge hilo, alisema wanapaswa kuachwa kwani
ni haki ya kila Mtanzania kutoa mchango wake ili kuwezesha kupatikana
Katiba mpya.
Filikunjombe
Said Juma Nkumba
“Hawa wazee wetu kina Jaji Joseph Warioba waache wazungumze na
waendelee kutoa maoni kwani wanayo haki hiyo,” alisema Dk Chegeni mmoja
wa makada vijana wa CCM.
Filikunjombe
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM),
amenukuliwa na kituo kimoja cha Televisheni nchini akisema kuwa haungi
mkono hatua iliyofikiwa na wajumbe wenzake wa CCM kuendelea na mchakato
wa Katiba Mpya kwa sababu suala la Katiba halina mshindi na pia ni
matumizi mabaya ya wingi wao ndani ya Bunge hilo.
Alipopigiwa simu na gazeti hili ili atoe ufafanuzi kuhusu kauli hiyo alisema: “Nitazungumzia hilo suala nikifika Dar es Salaam.”
Said Juma Nkumba
Kiongozi wa kundi la Tanzania Kwanza kutoka CCM,
Said Juma Nkumba alisema kitendo cha baadhi ya wabunge wa CCM kuelezea
misimamo yao ni ishara kwamba CCM haina msimamo katika hili.
“Hapo ndipo utaona kwamba CCM inazingatia
demokrasia ya watu au mtu binafsi, haiwezi kumzuia mtu kutoa maoni yake
kwani hiyo ndiyo demokrasia,” alisema Nkumba ambaye ni mbunge wa Sikonge
(CCM).
Aliongeza: “Suala hili la Katiba lina uhuru wa mawazo kwa kila mtu kusema chochote na ndiyo msingi wa demokrasia.”
Shinikizo la kutaka kusitishwa kwa Bunge hilo
lilianzishwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba Jumanne
iliyopita wakati akichangia mjadala wa mabadiliko ya kanuni.
Alilitaka Bunge Maalumu la Katiba lijitathmini
kama lina ulazima wa kuendelea wakati hakuna uhakika wa kupatikana kwa
theluthi mbili.
Alisema kitendo cha Bunge hilo kukaa kwa siku 84
bila uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa pande zote mbili
inayohitajika kupitisha Rasimu ya Katiba Mpya, hakiwezi kueleweka kwa
Watanzania.
Pia, akizungumza na gazeti hili juzi, Nchemba
alisema anaamini wapo wajumbe wengi kutoka CCM wanaomuunga mkono, ingawa
hawajapata nafasi ya kuzungumza.
TLS
LHRC
ACT-Tanzania
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
Alhamisi iliyopita alijibu akisema kauli ya Nchemba ni mtazamo wake
binafsi na hakuongea kama kiongozi wa chama hicho.
Wabunge wengine wa CCM waliotoa kauli za kumuunga
mkono Nchemba ni pamoja na Alli Keissy (Nkasi Kaskazini), James Lembeli
(Kahama) na Esther Bulaya (Viti Maalumu).
TLS
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS),
Charles Rwechungura alisema chama hicho kinafuatilia kwa makini kujua
athari za kuendelea kwa Bunge lenye wajumbe wa upande mmoja.
“Tunajiuliza je, endapo Katiba ikipatikana nini
athari zake kisiasa. Hapo ndipo tunakwenda mahakamani kuitaka Mahakama
itoe tafsiri ya vifungu vya sheria ili kujiridhisha uhalali wa Bunge
hilo kuendelea,” alisema Rwechungura.
Aliongeza: “Mahakama ikishagundua upungufu tutaiomba mahakama iusimamishe kwani utakuwa si halali na hauna tija kuendelea.”
LHRC
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo- Bisimba alisema baadhi ya
viongozi wanataka Katiba iliyopo ya mwaka 1977 iendelee kutumika.
“Wanauendeleza mchakato huu kwa lazima wakijua
kuwa kuna watu watakwenda mahakamani ili wapate kisingizio kwamba
tulitaka kuwatengenezea Katiba Mpya, lakini imezuiliwa,” alisema Dk
Bisimba
Aliongeza, “ Kitendo hicho ndicho
tunachokifuatilia kwa ukaribu, kwani Bunge hilo haliwezi kuendelea
wakati kundi fulani halipo.”
ACT-Tanzania
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT- Tanzania, Samson
Mwigamba alisema kuendelea kwa mchakato huo kama ulivyo inawezekana
ikapatikana Katiba Mpya yenye uhalali kisheria, lakini ikakosa uhalali
wa kisiasa au kijamii.
“Bunge Maalumu la Katiba lisimamishwe ili kuendelea kutoa fursa
ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka na maridhiano,” alisema Mwigamba.
Aliongeza: “Mchakato wa kuandika Katiba Mpya
uahirishwe hadi baada ya uchaguzi mkuu. Hivi sasa Bunge la Jamhuri
linatakiwa kufanya marekebisho katika Katiba ya sasa ili kuuwezesha
uchaguzi mkuu ujao 2015 uwe huru na wa haki.”
Baadhi ya maeneo ambayo Mwigamba aliyabainisha
kufanyiwa marekebisho kuwa ni; Tume ya uchaguzi iwe huru na ionekane
kuwa huru na kuruhusu mgombea binafsi na mbunge akitaka kuhama chama
ahame na ubunge wake.
Maeneo mengine ni: Kushuka kwa umri wa mgombea
urais, kuweka sharti kwamba ili mgombea atagazwe kuwa Rais lazima apate
angalau asilimia 50 ya kura zilizo halali na wagombea urais lazima
washiriki midahalo mitatu wakati wa kampeni.
Imeandaliwa na Ibrahim Yamola, Gooddluck Eliona (Dar) na Mussa Juma (Arusha). Source MWANANCHI
Mbunge wa Viti Maalumu, Chadema Leticia Nyerere akiwa kwenye viwanja vya bunge jana mjini Dodoma. Picha na Immanuel Herman
Dodoma. Mjumbe mwingine wa Bunge la Katiba kutoka Kundi la Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana alionekana kwenye Viwanja vya Bunge
na alisaini za mahudhurio.
Mjumbe aliyeonekana jana, Leticia Nyerere wa viti
maalumu, Chadema, anafanya idadi ya wajumbe waliotinga kwenye viwanja
hivyo hadi sasa kufikia watatu baada ya Chiku Abwao (viti maalumu
Chadema) kuonekana juzi na Clara Mwatuka (viti maalumu CUF) kuonekana
Jumapili.
Nyerere hakuwa akihudhuria vikao baada ya Ukawa kutangaza kususia Bunge mwezi Aprili na jana hakupatika kuzungumzia suala hilo.
Kuonekana kwa mjumbe hao kunaweza kutafsiriwa kuwa
ni kubomoka kwa ngome za Vyama vya Chadema, NCCR na CUF vinavyounda
umoja huo kwani tangu awali walikubaliana kutoshiriki shughuli za Bunge
hadi pale watakapofikia makubaliano ya hoja zao.
Msimamo wa chama hicho chini ya viongozi wao ni
kutohudhuria shughuli za Bunge Maalumu la Katiba hadi kutakapokuwa na
mwafaka wa mwenendo wa shughuli za chombo hicho, ambacho jana
kiliendelea na vikao vya kamati kujadili sura 15 za Rasimu ya Katiba.
Ukawa wanadai CCM imepora mawazo ya wananchi na
kwamba kuna mpango wa kuchakachua rasimu iliyotolewa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na kuingiza mambo yenye masilahi kwa chama hicho na
Serikali yake.
Vyama vinavyounda Ukawa vinadai kuwa kuzungumzia
muundo wa Muungano wa serikali mbili ni kuchakachua maoni ya wananchi
ambao walitaka muundo wa serikali tatu kama ilivyo kwenye Rasimu ya
Katiba.
Bunge jana lilikutana katika kamati zake 12
zilizotawanyika katika kumbi mbalimbali kwa ajili ya kupitia sura 15 za
rasimu ya Katiba ingawa wajumbe wengine walilazimika kuanzia safari zao
bungeni ili waweze kujisajili.
Mwenyekiti wa Kamati namba tano ambayo Nyerere ni
mjumbe, Hamad Rashid Mohamed alisema mjumbe huyo hakuwa amefika katika
kikao cha jana ambacho pia kilifanyika Dodoma Hoteli.
Kuhusu mwenendo wa kikao cha kamati yake, Mohamed
alisema hadi jana mchana walikuwa wamekamilisha kupitia sura ya pili na
kwamba jioni walitarajia kuifanyia kazi sura ya tatu.
Kuhusu changamoto ya muda, Mohamed alisema: “Hiyo
ndiyo hali halisi na tukiweza tutapiga kura kupitisha ibara hizo leo
(jana), kama tukishindwa basi tutapiga kura kesho (leo) ili mradi
tutumie muda ambao upo tufanye kazi kwa ufanisi.” Source MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment