Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta akizungumza na
wafugaji kutoka mikoa mbalimbali nchini walipomtembelea ofisini kwake
Dodoma jana. Wafugaji hao walipelekwa bungeni hapo na Mjumbe wa Bunge
hilo ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (kushoto).
Picha na Emmanuel Herman
Dodoma. Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta amesema mikutano ya Bunge hilo haiwezi kusitishwa na kwamba itaendelea kwa kuwa idadi ya wajumbe waliopo inakidhi matakwa ya kisheria kutunga Katiba.
Kadhalika Sitta amewatuhumu wajumbe wa wanatokana
na kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwamba si wazalendo
kutokana na kususia Bunge hilo tangu Aprili 25, mwaka huu.
Akizungumza na wafugaji kutoka mikoa mbalimbali
nchini walioongozwa na Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda
waliopeleka
mapendekezo yao ili yaingizwe kwenye rasimu ya
Katiba, Sitta alisema wanaotaka Bunge hilo liahirishwe ni watu
wasiolitakia mema Taifa.
“Lakini napenda kuwaambia kuwa Bunge la Katiba
liko hapa kisheria kwa kanuni zake linaendelea na wale wanaopiga kelele
lisiendelee ni watu ambao hawatutakii mema,” alisema Sitta na kuongeza;
“Kwa sababu demokrasia yoyote ni kupata kura za
wengi, walioko hapa wanatosha kabisa kuendelea na mchakato huu mpaka
mwisho wake kwa sababu tunaamini wakati wa Katiba Mpya umefika.”
Kauli ya Sitta imekuja siku moja tangu viongozi wa
Ukawa unaojumuisha vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF watangaze
kwamba wataitisha maandamano nchi nzima kushinikiza kusitishwa kwa Bunge
hilo kwa maelezo kwamba ni matumizi mabaya ya fedha za umma iwapo Bunge
hilo halitasitishwa.
Kadhalika, baadhi ya wabunge wa CCM wamesikika
wakitaka Bunge hilo liahirishwe ili kunusuru fedha zinazotumika
kugharamia shughuli zake, kwani hakuna uhakika wa kupatikana kwa
theluthi mbili ya kuwezesha Katiba hiyo kupatikana.
Sitta alisema hakuna ubishi kwamba baadhi ya
wajumbe walitoka ndani ya bunge hilo na kwenda nje ambapo wamekuwa
wakipiga kelele na kwamba wao (waliobaki bungeni) ambao wana uzalendo
lazima wahangaike nayo mpaka iweze kupatikana.
Alisema upungufu uliopo katika Katiba ya sasa,
ndiyo unaofanya kutotungwa kwa sheria bora ambazo zitawezesha maslahi ya
makundi mbalimbali yapatikane bila kuleta migongano kama iliyopo sasa.
“Ndio maana sisi tunasema kung’ang’ania suala la
muundo wa serikali ni kwenda pembeni kidogo na matarajio ya watu. Huu ni
ushahidi dhahiri kabisa kuwa lililo muhimu ni haki za raia,” alisema.
Alisema hata kama Katiba itakuwa na muundo wa
serikali kwa idadi yoyote, ikiwa haitazingatia haki za makundi kama
wafugaji, haitakuwa na maana.
Sitta alisema wanaifanyia kazi Katiba hiyo na kuwa itakuwa bora zaidi kushinda nyingine zilizopo katika nchi jirani.
Shibuda akandia Ukawa
Kwa upande wake Shibuda ambaye pia ni alijiita
mlezi wa wafuhaji, aliwakandia Ukawa akisema wamekuwa wakitanguliza
maslahi binafsi badala ya maslahi ya Wananchi huku akimpongeza Sitta kwa
jitihada za kuendeleza mchakato wa Katiba.
“Napenda vile vile kukupongeza kwa jitihada zako
za kuendeleza mchakato huu, pia nikupe pole kwa visirani vya kusigana
vinavyotokea,” alisema Shibuda ambaye hata hivyo hakutamka moja kwa moja
iwapo amerejea kushiriki vikao vya Bunge Maalum.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema: “Subirini mtaona yatakayojiri”.
“Wafugaji na wakulima wa pamba wanalaani na
kusikitika kwamba Bunge hili linaacha kujadili matatizo yanayoikabili
jamii badala yake ajenda muhimu inakuwa mfumo wa madaraka,” alisema na
kuongeza;
“Hivi serikali tatu inatiririsha nini kwa
wakulima? Serikali mbili inatiririsha nini kwa wakulima na wafugaji?
Tunataka uongozi wa kukabiliana na matatizo ya wananchi, sio uongozi wa
kukimbia matatizo ya wananchi.”
Shibuda alisema wakulima na wafugaji wanahitaji
siasa iwe ni rufaa ya kujenga maendeleo ya jamii na kujengwa ukombozi wa
Watanzania.
Shibuda alisema wao hawatakubaliana na watu wanaotaka kukuza umaarufu binafsi.
“Mimi nitapingana na mtu yoyote, nitakwenda kwenye
jamii, nitakuja kwenu wafugaji nitakwenda kwa wakulima wa pamba ambao
mimi ni mlezi wao, tutashauriana tukatae kutumiwa na kuburuzwa na
maslahi ya watu wanaotaka kujikweza kwa maslahi binafsi,” alisema.
Alisema wakulima na wafugaji hawakubaliani na
kauli za kibabe za watu wachache ambao wanategemea kutoa uhuru wa maoni
yao kutegemea Katiba ya nchi lakini wakitofautiana mitazamo wanaanza
kuwa wababe wanaoitwa chinjachinja kwa watu ambao wanatoa mawazo
mbadala.
“Mheshimiwa (Sitta) wasikutishe kwa dhamira yako
njema ya kuongoza vikao, hakuna chema kisicho na kasoro, mtu kama ana
dhamira njema akiona kasoro akusahihishe kwa lugha ya kistaarabu kwa
maslahi ya kusonga mbele,” alisema.
Akisoma mapendekezo ya wafugaji hao, Mwenyekiti wa Chama cha
Wafugaji wa Kanda ya Magharibi, Kasundwa Wamarwa alisema wanatambau kuwa
Bunge hilo litawapatia Katiba inayowatambua wafugaji wa asili.
“Kwa kauli moja sisi wafugaji hatutakuwa tayari kuipokea rasimu ya Katiba ambayo haitatambua mfugaji wa asili,” alisema.
Alisema njia kuu ambayo wanaamini itakuwa
suluhisho ya matatizo yao ni Katiba Mpya huku akisema wajumbe wa Bunge
la Katiba wanapaswa kuwa na hofu ya Mungu wakati wanapoendelea na
mchakato huo.
“Tunawataka wajumbe wa Bunge la Katiba kukumbuka
kuwa Katiba bora ni ile itakayotokana na maridhiano na utashi wa
kisiasa,” alisema. Chanzo MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment