
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza mwanafunzi wa kidato cha
nne Neema Steven Mtwanga(16) anayesoma katika shule ya sekondari Naboti
Makambako,Njombe baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika utunzi wa
insha katika shindano lililoandaliwa na Jumuiya ya uchumi ya maendeleo
kusini mwa Afrika(SADC).Rais Kikwete alimpongeza mwanafunzi huyo wakati
wa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa wakuu wa nchi za SADC
unaofanyika katika mji wa kitalii wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe
ambapo mwanafunzi huyo aliandika insha inayohusu mabadiliko ya tabia
nchi.

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete(kulia) akiwa katika picha ya pamoja na
wakuu na wawakilishi wa nchi za Jumuiya ya uchumi kusini mwa Afrika
SADC muda mfupi baada ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa jumuiya hiyo
uliofanyika katika hoteli ya Elephant Hills mjini Victoria Falls
Zimbabwe leo.Katikati ji mwenyeji wa Mkutano huo Rais Robert Mugabe na
Dkt Stergomena Tax [katibu mkuu wa SADC] na kwa upande wake wa kushoto
ni Nkosazana Dlamini-Zuma (Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika)
Msichana Neema Steven Mtwanga, 16, kutoka Shule ya Sekondari ya Naboti, Mkoa wa Njombe, ametunukiwa Tuzo ya ushindi huo katika Mkutano wa 34 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC ulioanza leo katika Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria Falls, Zimbabwe.
Nafasi ya pili imeshikwa na Kudzai Ncube kutoka Shule ya Sekondari ya Mazowe nchini Zimbabwe na nafasi ya tatu imeshikwa na Manxoba Msibi kutoka Shule ya Sekondari ya Etjendlovu katika Swaziland.
Kwa ushindi huo, Neema Steven Mtwanga ambaye yuko kidato cha nne, amezawadiwa hundi ya dola za Marekani 1500 ambayo ni sawa na shilingi milioni 2.3 na amelipiwa gharama zote za kumwezesha kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC na kukabidhiwa zawadi hiyo. Aidha, Neema amepewa zawadi ya ipad kwa ajili ya matumizi yake ya teknolojia ya mawasiliano na habari.
Mashindano hayo ya Insha ya Mwaka 2014 yalianzishwa rasmi Oktoba, 2013 ambako washindani walitakiwa kuandika Insha kuhusu mada: “Climate Change is having adverse effect on the socio-economic development in the Region. What should the Education Sector do to mitigate the impact on the youth” – Mabadiliko ya Tabia Nchi yanaathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Kanda ya SADC. Nini Sekta ya Elimu ifanye kupunguza athari hizo kwa vijana?
Insha 39 zilipokelewa kutoka nchi 13 kati ya nchi 15 wanachama wa SADC ikiwa ni Insha tatu kwa kila nchi. Insha zilipokelewa kutoka Tanzania, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Lesotho, Malawi, Mauritius, Mozambique, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Zambia na Zimbabwe.
Majaji wa kupitia na kuamua washindi wa Insha hizo walitoka Tanzania, Zambia na Zimbabwe na walikutana mjini Gaborone, Botswana, Julai, mwaka huu kupitia Insha zote na kutoa uamuzi wa nani washindi.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo wa SADC umepokea kwa furaha
ushindi wa msichana Neema ukieleza kuwa ushindi huo umeiletea Tanzania
heshima kubwa katika eneo la SADC na nje ya eneo hilo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
17 Agosti,2014
0 comments:
Post a Comment