Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,Samuel Sitta. PICHA |MAKTABA
Na Neville Meena,Mwananchi
Dodoma. Wakati kamati za Bunge
Maalumu zikiendelea na uchambuzi wa Rasimu ya Katiba, mwelekeo wa kuzika
muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba
umejidhihirisha huku mabishano yakitawala katika baadhi ya kamati kuhusu
suala hilo.
Jana, baadhi ya kamati hizo zilianza kujadili sura
namba 7, 8, 11, 14 na 15 ambazo zinagusa masuala kadhaa yanayohusu
muundo wa muungano, huku zikigawa baadhi ya majukumu kwa serikali za
nchi washirika – Tanganyika na Zanzibar.
Habari kutoka katika baadhi ya kamati zinasema
baadhi ya maneno kama vile ‘serikali za nchi washirika na Rais wa
Tanganyika yamependekezwa kufutwa, huku baadhi ya wenyeviti wakisema
wanajadili sura hizo kwa kuzingatia mapendekezo yao ya awali.
Tayari kamati zote zilishajadili sura namba moja
na sita zinazohusu muundo wa muungano na nyingi zilipendekeza kuendelea
kwa muundo wa serikali mbili, lakini uamuzi wa mwisho haujafanyika
katika Bunge hadi sasa kutokana na mvutano ulioligawa kuhusu suala hilo.
Kamati namba moja inayoongozwa na Naibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Makamu Rais, Ummy Mwalimu imependekeza kuundwa kwa sura
maalumu ya ardhi na rasilimali ili kuondoa migogoro ya wakulima na
wafugaji.
Sura hiyo haimo kwenye Rasimu ya Katiba kwani Tume
ya Mabadiliko ya Katiba ilipendekeza suala hilo kuwa chini ya serikali
za nchi washirika.
“Kamati iliona kwamba kuna changamoto
zinazowakabili wakulima na wafugaji, tukaamua tuwe na sura mpya ya ardhi
ambayo itazungumzia masuala ya ardhi,” alisema Mwalimu.
Kuhusu hoja kwamba kufanya hivyo ni kwenda nje ya
Rasimu ya Katiba iliyoacha suala hilo mikononi mwa nchi washirika,
Mwalimu alisema kamati yake inachambua sehemu za rasimu zilizobaki kwa
kuzingatia mapendekezo yake ya awali ya muundo wa muungano wa serikali
mbili.
Juzi, kamati ya wajumbe wanaowakilisha wakulima,
wafugaji, wavuvi na wachimbaji wadogo wa madini waliwasilisha kwa Katibu
wa Bunge Maalumu mapendekezo ya sura mpya inayohusu masuala ya ardhi,
maliasili na mazingira.
Mmoja wa wajumbe hao kutoka kundi la wakulima,
Hamis Dambaya alisema walichukua hatua hiyo kutokana na makundi hayo
kutokutajwa kwa kina katika Rasimu ya Katiba.
“Tuliwasilisha mapendekezo yetu kwa Katibu jana
(juzi) na leo (jana) tumeambiwa kwamba kuna Kamati ya Uongozi, hatujui
pengine huenda yakajadiliwa na kuruhusiwa kupelekwa kwenye kamati zote
kwa ajili ya kujadiliwa,” alisema Dambaya.
Ndani ya Kamati
Wakati hayo yakiendelea, katika kamati namba 11 inayoongozwa na
Anne Kilango Malecela kuliripotiwa kwamba hawakuwa wamekubaliana kuhusu
kufutwa ama kuachwa kwa maneno yenye mwelekeo wa kutaja serikali tatu.
Suala hilo lilizua mjadala na baadaye mvutano
mkali pale wajumbe walipotaka kurekebisha baadhi ya vifungu ili viwe na
mwelekeo wa mfumo wa serikali mbili, huku uongozi wa kamati hiyo ukisema
kuwa uamuzi kuhusu suala hilo ulishaafikiwa awali.
“Tuliwauliza uamuzi upi ulishafikiwa wakati
hatujapiga kura? Wakajibu kuwa utaratibu umebadilika kwamba hakuna
kupiga kura ila michango ya watu wengi ndiyo uamuzi, kwa hiyo sisi
tumekaa kimya tunasubiri kuona, ila kweli hatutakubali,” alisema mmoja
wa wajumbe wa kamati hiyo.
Kwa upande wa Kamati namba tano, habari zinasema
wajumbe wameamua kuacha maneno kama yalivyo ili kuepuka kuwaudhi wajumbe
wenye mitazamo inayokinzana.
“Kama mahali pameandikwa Tanganyika tunaacha
hivyohivyo, maana sasa tukisema tufute itakuwa shida kwa sababu kwenye
kamati yetu wamo wajumbe wanaounga mkono serikali tatu na kama unavyojua
Bunge halikupiga kura kuamua jambo hili,” alisema mmoja wa wajumbe wa
kamati hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati namba tisa, Kidawa Himid Salehe, alisema hawajadili muundo wa serikali tatu wala mbili kwa sababu zilishajadiliwa katika sura namba moja na namba sita.
Akizungumza katika viwanja vya Bunge jana, Kidawa alisema kinachojadiliwa ni msingi wa kile kichopo katika sura husika.
Hata hivyo, alisema kuwa wamepokea mapendekezo ya
ibara nyingine katika sura ambazo wamezijadili. Kidawa alisema baadhi ya
mapendekezo ni yale yanayohusu masuala ya ardhi kutoka kwa makundi ya
wawakilishi wa wakulima na wafugaji. Chanzo MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment