Doroth Myunga akionyesha bidhaa zake katika maonyesho ya Nanenane
yaliyofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya hivi
karibuni. Picha na Hawa Mathias
Mbeya. Ni katika Viwanja vya Maonyesho ya Nanenane vya John
Mwakangale jijini Mbeya ndipo mjane Doroth Myunga anaeleza machungu ya
maisha aliyokumbana baada ya kufiwa na mume wake mwaka 2005.
Anasema kuwa ugumu wa maisha aliokumbana nao
ulimfanya apate akili ya kujikita katika kilimo kwa mtaji wa Sh1.3
milioni, baada ya kuuza ng’ombe mmoja aliyeachiwa kama urithi na
marehemu mumewe.
Doroth alihitimu elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Igula, Tarafa ya Isimani.
Kata ya Kihorogoto mkoani Iringa Mwaka 1989,
lakini hakupata fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na
kukosa msaada wa kuendelezwa kwani wazazi wake hawakuwa na uwezo.
Anaeleza kuwa mbali na kujikita katika kilimo,
amekuwa akijihusisha pia na ujasiriamali wa kutengeneza urembo wa
mapambo ya nyumbani ofisini kwa kutumia shanga ili kujipatia fedha.
Anasema kuwa bidhaa hizo za urembo amekuwa akiziuza kwa kati ya Sh50,000 hadi Sh150,000 kulingana na mahitaji ya wateja wake.
Doroth anasema kuwa kutokana na shughuli za
ujasiriamali, ameweza kujipatia Sh,300,000 kwa siku, fedha ambazo
zinamsaidia kujikimu na hali ya maisha licha ya kujikita katika kilimo
pia.
Anasema kuwa ujane alionao haukumfanya kukata
tamaa ya maisha, bali aliendelea kupambana na kujikita zaidi katika
kilimo na kuhamasisha wanawake wengine kijijini kuanzisha kikundi na
kuwa na shamba la mfano, ambalo kwa kiasi kikubwa lilimekuwa mkombozi.
“Tumeweza kulima alizeti na kupata magunia 18 ambayo tuliuza na kupata zaidi ya Sh2 milioni za kikundi,”anasema.
Anabainisha kuwa walianza kukopeshana fedha hizo
kwa kila mwanachama kupata Sh200,000 hali iliyompatia mwanga kuwekeza
zaidi katika kilimo na kutokana tamaa.
Anaeleza kuwa kutokana na mtaji huo kwa msimu huu
wa kilimo amefanikiwa kupata magunia 40 ya alizeti ambayo anatarajia
kuuza ili aweze kuboresha zaidi maisha yake.
Doroth anasema kuwa kilimo kimempa mafanikio
makubwa na kwamba mpaka sasa ameweza kumiliki trekta lenye thamani ya
Sh39 milioni, hali iliyomwezesha kuachana na kilimo cha jembe la mkono
na kulima kisasa hivyo kujikuta akipata mazao mengi zaidi.
Mwanamke huyo anasema kuwa matarajio yake ni kujenga nyumba ya
kisasa kujikita katika usindikaji wa zao la alizeti kwa kuchuja mafuta
na kutafuta zabuni ya kusambaza mashudu kwa wananchi wanaojihusisha na
ufugaji.
Doroth anabainisha kuwa wameweza kupata mikopo
mbalimbali katika kikundi chao kupitia katika Halmashauri ya Mji wa
Iringa kwa lengo la kuboresha kilimo cha mazao ya chakula na biashara
hasa kwa wajane walio vijijini.
Wito
Doroth anatoa wito kwa wanawake kuwa wasichukulie
hali hiyo kuwa ni sababu ya kubweteka na kukimbilia kuolewa au
kulalamika, badala yake wajitume katika shughuli mbalimbali za kijamii
hasa kuanzisha miradi midogo ya ujasiriamali ili kujiopatia fedha na
kutunza familia zao wakiachana na dhana ya kurithiwa au kuolewa tena.
“Ujane isiwe changamoto kwa wakinanamama bali ni
kupambana na maisha kwa kujishughulisha na kilimo na kuanzisha miradi ya
ujasiriamali ili kujikwamua kiuchumi,”anasema.
Doroth anasema kuwa wakati umefika kwa wajane kuwa
katika vikundi ili Serikali iweze kuwatambua na kuwapatia mikopo yenye
riba nafuu ili kuweza kujinasua katika hali duni ya masha na utegemezi
katika familia.
Anaweka wazi kuwa binafsi aliwahi kushiriki
Shindano la Mama Shujaa wa Chakula mwaka 2012, ingawa hakufanikiwa
kupata nafasi, lakini hakati tamaa akiamini ipo siku atafanikiwa kwani
yeye ni mkulima hodari.
Changamoto
Anasema kuwa wakulima wa vijijini wamekuwa na
changamoto ya ukosefu wa miundombinu mizuri ya barabara, maji na nishati
ya umeme hali inayosababisha kutofikia ndoto zao za usindikaji wa mazao
wanayozalisha.
Anaiomba Serikali kuwezesha wakulima wa vijijini
kwa kuhakikisha wanafikiwa na wataalamu wa kilimo ili kuboresha kilimo
kilicho na tija na kupata soko la ndani na nje ya nchi pamoja na kupata
pembejeo za kilimo hususan matrekta madogo.
Doroth anaomba wadau mbalimbali nchini kusaidia
kutetea haki za wajane akisema kundi hilo limekuwa na changamoto kubwa
ya kuporwa mali wanazoachiwa na waume zao wanapofariki. Chanzo MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment