Sunday, 17 August 2014

Mchakato wa Katiba Mpya ukisitishwa...

UPO uwezekano mkubwa – kama kwa lazima au kwa kukosa njia nyingine – mchakato wa Katiba mpya utasitishwa.

Uwezekano huu upo kwa sababu ya kutokuwapo maridhiano yenye kuwezesha majadiliano kuendelea katika Bunge Maalumu la Katiba kufikia uandikwaji wa Katiba inayopendekezwa.

Uwezekano wa kusitishwa kwa mchakato huu umepata nguvu zaidi siku za karibuni hasa baadhi ya wanasiasa kutoka chama tawala wanapotoa mawazo ya kutaka mchakato huu usitishwe hasa kwa vile hakuna maridhiano kati ya wajumbe wanaotokana na Chama cha Mapinduzi (CCM) na wale wanaotokana na wajumbe wa kundi la UKAWA lenye kujumuisha vyama vikuu vya upinzani nchini kama CUF, CHADEMA, na NCCR Mageuzi.

Kama hili ni kweli – na ninaamini lina ukweli – basi ni lazima tujiulize na kutafuta jibu au majibu ya ni nini kinapaswa kutokea endapo mchakato huu utasisishwa.

Ni muhimu kujua mambo mbalimbali yanayopaswa kutokea ili tusije kujikuta tunarudia tena gotagota hii miaka michache ijayo.

Mchakato usiahirishwe, usitishwe tuanze moja

Jambo la kwanza na la msingi endapo uamuzi wa kusitisha mchakato huu utachukuliwa ni kuhakikisha kuwa uamuzi wowote hautakuwa wa kuahirisha kama vile kuahirisha kikao cha Bunge la Muungano au Baraza la Wawakilishi.

Kuahirisha kwa namna fulani itakuwa ni sawa na kukubali kwa kiasi fulani yale yaliyotokea na kuwa tutaendelea “kuanzia tulipoishia”.

Kwa maoni yangu, mchakato huu ulivurugwa tokea mwanzo kabisa na hivyo hata kuukubali kwa kidogo ni kuupa heshima isiyostahili.

Ni vizuri basi uamuzi uwe wa kuufuta kabisa na kile kilichokwenda kwa mganga (kilicholiwa) tukubali kuwa kimeliwa kwa sababu ya ubishi na kiburi chetu kama Taifa.

Tuufute mchakato huu na kuacha uongozi ujao au vizazi vijavyo vianzishe mchakato wao. Sisi tumejaribu pamoja na elimu na ujuzi wetu lakini ndiyo tumeboronga hivi labda kipo kizazi cha wenye weledi, akili, uzalendo na fikra bora ambacho kitafuata njia sahihi za kuelekea Katiba mpya.

Tusubiri tuone kuelekea kampeni za uchaguzi ni chama gani au vyama gani vitakuja na ajenda inayoeleweka kuhusiana na Katiba mpya.

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ifutwe

Kwa vile mchakato huu umekuwa ukiendeshwa kwa kufuata ile sheria mbovu ya Mabadiliko ya Katiba, basi hakuna njia nyingine ya kuusitisha isipokuwa kwa kufutilia mbali sheria ile ambayo ilitungwa ikiwa inapingana na Katiba ya sasa kwa asilimia 100. Nimeshawahi kuonyesha jinsi mchakato huu ulivyokuwa haramu na sehemu mojawapo ya uharamu huo ni hii sheria.

Ni vizuri basi hoja itakapotolewa kuusitisha mchakato huu wabunge wetu wa Bunge la Muungano wajiandae kuleta mswada wa sheria itakayofutilia mbali sheria hii na hivyo kuhakikisha kuwa mchakato huu unakufa kifo cha asili ili tusije kuwaachia viporo na mabaki yanayonuka wale wanaotaka kuja na kuanzisha mchakato mpya wa katiba mpya.

Hatima ya Muungano iamuliwe kabla ya Katiba mpya

Hili likitokea – kufutiliwa kwa mchakato huu- mambo ya msingi sasa ni lazima yashughulikiwe mapema iwezekanavyo ili angalau kwa kiasi kikubwa kupunguza kazi huko mbele.

Baadhi ya mambo ambayo yanahitaji kushughulikiwa mapema zaidi tena chini ya Katiba sasa ni suala zima la kuwapo kwa Muungano.

Kati ya matatizo ambayo tayari tumeyaona na yalikuwa yanatabirika sana tu ni nafasi ya Zanzibar katika Muungano wa sasa na nafasi ya Tanganyika katika Muungano mpya.

Haya mawili yamekuwa sehemu ya matatizo yetu ya kisiasa kwa muda mrefu sasa na wakati umefika yaamuliwe mapema zaidi na ikiwezekana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Suala la Muungano limekuwa tatizo kwa muda mrefu kwa sababu ya Zanzibar. Wakati umefika kwa Wazanzibari kuamua kama wanataka kuwa sehemu ya Muungano na Tanganyika.

Tokea mwanzo kabisa wa Muungano wetu Zanzibar imekuwa ikipewa upendeleo na nafasi ya pekee kulinganisha na Tanganyika. Kwa Watanganyika wengi uwepo au kutokuwepo kwa Zanzibar katika Muungano si hoja nzito kwao.

Lakini uwepo wa Tanganyika kwa nchi ya Zanzibar ndani ya Muungano ni jambo kubwa. Hofu ile ambayo ilikuwepo toka mwanzo kwamba katika Muungano itaonekana Tanganyika imeimeza Zanzibar imeshatimia na imekuwa kweli.

Hoja zote tunazosikia kuhusu “Mamlaka Kamili” na “Zanzibar Kwanza” yote ni matokeo ya ukweli huu kuwa Zanzibar inajihisi au angalau tuseme lipo kundi linaloamini Zanzibar imemezwa na Tanganyika na sasa wanataka kujitoa katika koo hilo.

Kama hili ni kweli au la ni Wazanzibari tu wanapaswa kuamua. Ni maoni yangu kuwa wakati umefika kwa Wazanzibari kama walivyofanya kwenye suala la Serikali yao ya “Umoja wa Kitaifa” na mabadiliko ya Katiba yao waanze kudai mapema iwezekanevyo si tena “mamlaka kamili” bali “Kura ya Maoni” ili kujitoa kwenye Muungano.

Wao tayari wana vyombo vyote vinavyoweza kusimamia hili na sioni sababu ya msingi kwanini wasifanye hivyo.

Imetosha kusikia malalamiko na manung’uniko. Wazanzibar wadai wapatiwe nafasi ya kupiga kura ya maoni kama wanataka kuendelea kuwa sehemu ya Muungano au la.

Kama watasema hawataki basi uwekwe utaratibu ni lini na tarehe gani Zanzibar itarudi na kuwa nchi huru yenye mamlaka kamili (secede from the Union). Hili litasaidia hata siasa za Tanganyika kwani mazungumzo ya Tanganyika yataacha kufikiria namna ya kuwaridhisha Wazanzibari na badala yake watazungumzia namna ya kuipatia Tanganyika Katiba yake na vyombo vyake vya utawala ambavyo vingi kama si vyote viko katika “Serikali ya Muungano” hivi sasa.

Haya ni mambo makubwa na ya msingi kutokea na yanapaswa kutokea mapema iwezekanavyo. Hii ni pamoja na mabadiliko ya msingi ya Katiba ya sasa ili kusaidia michakato mbalimbali ya kisiasa katika mazingira bora kama katika Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama siasa n.k.

Tukifikia huku basi tutakuwa tumefika mahali pazuri na nina uhakika tutarahisisha sana kazi ya kuandika Katiba mpya – ama iwe ya Muungano au ya Tanganyika – huko mbele. Tufanye mambo ya msingi kwanza.

Makala hii imenukuliwa kutoka gazetini: Raia Mwema

0 comments:

Post a Comment