Mhe. Waziri Bernard K. Membe (MP), Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, akiongea na waandishi wa habari katika Ofisi
za Wizara ya Mambo ya Nje. Kulia ni Balozi Vincent Kibwana, Kaimu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mhe. Waziri aliyasema hayo alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam
“Serikai haikumfukuza mkimbizi yeyote isipokuwa iliwafukuza wahamiaji
haramu, Aidha, wahamiaji haramu hao walipewa onyo la kuondoka nchini na
wengi wao wametii kabla ya operesheni maalum ya kuwatia mbaroni
haijaanza” Waziri Membe alisikika akisema.
Kuhusu hoja kuwa operesheni ya kuwafukuza wahamiaji haramu inawalenga
Wanyarwanda, Waziri Membe alisema kuwa hoja hiyo sio ya kweli. Alisema
kuwa hadi kufikia wakati huu zaidi ya wahamiaji haramu 31,000 wameondoka
nchini. Kati ya hao Warundi ni 21,000, Wanyarwanda ni 6,000 tu na
waliobaki ni kutoka nchi nyingine..
Mhe. Membe aliwaambia waandishi wa habari kuwa Tanzania imekuwa
kimbilio la wakimbizi kwa muda mrefu na hadi sasa inahifadhi wakimbizi
zaidi ya laki 4. Wakati wote wakimbizi wamekuwa wakipewa huduma nzuri na
haijawahi kusikika kuwa Tanzania inalaaniwa na Shirika la Wakimbizi la
Umoja wa Mataifa au Jumuiya ya Kimataifa kwamba Serikali inawanyanyasa
wakimbizi.
Sambamba na taarifa hiyo, Mhe. Waziri aliwaambia waandishi wa habari
kuhusu mikutano inayofanywa na baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki (Kenya, Uganda na Rwanda) bila kuhusisha nchi nyingine
wanachama wa jumuiya hiyo.
Mhe. Membe alisema kuwa yeye binafsi hana tatizo na mikutano hiyo
endapo tu, imepata kibali cha Wakuu wa Nchi wa EAC pamoja na kutoa
ripoti ya masuala yanayozungumzwa katika vikao vya jumuiya. “Mimi
binafsi sioni tatizo kwa nchi hizo kukutana endapo zimepewa Baraka na
Wakuu wote wa Nchi wa EAC na ripoti za mikutano yao kuwasilishwa katika
vikao rasmi vya jumuiya” alisema Mhe. Membe.
Aliwatoa shaka Watanzania kutokuwa na hofu na mikutano hiyo kwa kuwa
Tanzania ni nchi muhimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo
hainabudi nchi nyingine kuitegemea kutokana na rasilimali zilizopo na
jiografia yake.
Alihitimisha mazungumzo yake kwa kusema kuwa anaamini vikao
vinavyofanywa, vinafanywa kwa nia njema pasipo kuwa na dhamira ya kuleta
mgawanyiko ndani ya jumuiya. Na endapo vinafanywa kwa dhamira ya kuleta
mgawanyiko basi muda wa kurekebisha hali hiyo upo.
0 comments:
Post a Comment