Mshambuliaji
wa zamani wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Joseph Kaniki
amepandishwa kizimbani jijini Addis Ababa, Ethiopia kutokana na tuhuma
za kukamatwa na madawa ya kulevya.
Iwapo
Kaniki pamoja na mwenzake Mkwanda Matumla ambaye ni bondia watapatikana
na hatia, basi watafungwa nchini Ethiopia hadi watakapomaliza kifungo
chao, Serikali ya Tanzania imethibitisha hilo.
Kaimu
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Samuel Shelukindo ameliambia
Championi Ijumaa, jana kutoka Addis Ababa kuwa, Kaniki na Mkwanda
walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa wiki na huenda ikawa hivyo tena wiki ijayo.
“Jana
(juzi) tulikwenda kuwaona na tumekuwa tukifuatilia kwa karibu, huku
kidogo kuna utaratibu tofauti, hivyo hatujajua lini watapandishwa tena
kizimbani kwa mara ya pili.
“Iwapo
watapatikana na hatia, kama ni kifungo cha jela, basi watatumikia hapa
Ethiopia. Maana tunabanwa kutokana na kutokuwa na mkataba wa kupeana
washitakiwa au wafungwa kama ambavyo nilieleza awali,” alisema
Shelukindo.
“Hii
juzi tu, kuna Watanzania wengine walikuwa wamefungwa hapa na tayari
wameshamaliza vifungo vyao, wameondoka kurejea nyumbani.
“Lakini
tumekuwa tukifuatilia kwa karibu, lengo ni kuhakikisha hata kama
watuhumiwa au wakihukumiwa, basi haki yao inapatikana. Uingereza,
Marekani na nchi nyingine wamekuwa wakifanya hivyo.”
Lakini
taarifa nyingine ambazo gazeti hili limezipata kutoka kwa Mtanzania
anayeishi Addis Ababa, zinaeleza Kaniki amekuwa akilia gerezani usiku
kucha.
“Kuna
Watanzania wenzetu wamefungwa katika gereza ambalo Kaniki yumo,
tulienda kuwaona juzi, yeye hatukumuona. Ila wanasema amekuwa akilia
usiku kucha, tena wakati mwingine kwa sauti ya juu akionekana kulijutia
suala hilo,” alisema Mtanzania huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake
gazetini.
Kaniki
na Mkwanda walikamatwa siku kadhaa zilizopita kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Bole, Addis Ababa nchini humo wakiwa njiani kwenda barani
Ulaya na taarifa zinaeleza wangetua Italia, nyingine Hispania lakini
wawili hao wanaishi Sweden.
Kaniki
amewahi kuzichezea Simba, Mtibwa Sugar na Rayon Sports ya Rwanda,
alikwenda kufanya majaribio Sweden ambako alifeli lakini baadaye
akasajiliwa na timu ya daraja la pili ya Konya ambayo hata hivyo,
hakudumu nayo na kazi yake ya mwisho ilikuwa ni ufagizi katika kampuni
ya usajili mjini Norrkoping.
CHANZO: GAZETI LA CHAMPIONI
0 comments:
Post a Comment