KAMPENI ya kitaifa ya kuondoa wahamiaji haramu nchini iliyopewa jina la Operesheni Kimbunga, imefanikiwa kusambaratisha kijiji cha wahamiaji haramu wa Burundi waliokuwa wamejitengenezea dola yao nchini, kiasi cha
hata kutumia sarafu ya Burundi ilihali wakiwa Tanzania.
Aidha, watoto wao wanasoma shule kwa mitaala ya Burundi, ikiwa ni pamoja na kuwafundisha kwa lugha ya Kifaransa wakiwa kijijini Nyamugali, Mvugwe wilayani Kasulu, Kigoma.
Hayo yamethibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, Issa Machibya katika mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake mjini hapa.
Kutokana na hatua hiyo, baadhi ya wakazi wa mkoani Kigoma, wakiwemo wa Manispaa ya Kigoma Ujiji na wilaya za Kasulu na Buhigwe, wamepongeza hatua hiyo.
Wameitaka serikali kutorudi nyuma katika kuhakikisha inawaondoa nchini wahamiaji haramu ambao wametajwa kuwa tishio kwa usalama wa nchi kutokana na kujihusisha na matukio ya ujangili, biashara ya silaha zikiwemo za kivita, na matukio mengine.
Akizungumza mjini hapa, Machibya alisema mbali ya kutumia faranga (fedha za Burundi) kwa matumizi yao ya kawaida wakiwa nchini na kufundisha kwa mitaala ya nchi waliyotoka, wahamiaji hao walipeperusha pia bendera ya nchi yao katika sehemu mbalimbali za kijiji hicho.
“Lakini kwa sasa, wote wamekimbia na kuziacha nyumba zao. Huwezi kuamini kama ni nyumba za wahamiaji haramu, kwani walijijenga na kuishi watakavyo, tena bila ya hofu katika nchi ya kigeni.
“Hebu tafakari, ni dharau gani unaishi Tanzania, lakini hata pesa yao hutumii, badala yake unatumia faranga.Tunashukuru tumewasambaratisha, na tutaendelea na operesheni hii mpaka tuhakikishe Watanzania
wanaishi kwa amani katika ardhi yao,” alisema Machibya.