Baadhi
ya Wajumbe wanawake wa Bunge Maalum la Katiba wakiimba kwa furaha
wakati wa semina iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
Makamu
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba (wa kwanza kulia) akipitia taarifa
ya mapendekezo ya mtandao wa wanawake na Katiba Tanzania wakati wa
semina iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
Mjumbe
wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Bi. Usu Mallya akitoa mada kuhusiana
na suala la kijinsia katika Katiba, wakati wa Semina iliyoandaliwa na
Umoja huo kwa kushirikiana na Mtandao wa Wanawake na Katiba kwaajili ya
Wajumbe wa Bunge Maalum kuhusu masuala ya Jinsia na Katiba iliyofanyika
kwenye Ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa Mjini Dodoma.
Usawa wa jinsia ni hali ya wanawake na wanaume kuwa na fursa sawa na
upatikanaji wa haki zenye kuleta tija katika Nyanja mbalimbali za
maendeleo ya jamii.Kati ya makundi haya mawili, lengo kuu la kuwepo kwa
usawa wa jinsia ni kuhakikisha kuwa raia wote wanapewa nafasi ya kukua
na kuondolewa vikwazo mbalimbali ili waweze kuchangia na kutambuliwa kwa
usawa katika maendeleo yao ya kijamii, kiutamaduni, kiuchumi pamoja na
kisiasa.
Ili Katiba iwe yenye mrengo wa jinsia
hainabudi iwe inayotokana na mchakato uliyoshirikisha sauti za wanawake
na wanaume wakati wa uandaaji wake na pia iliyoweka bayana makubaliano
ya misingi mikuu itakayoongoza nchi ikibeba sauti zao.
Sambamba
na hilo, Katiba hainabudi kuzingatia misingi ya demokrasia ikiwemo
utawala wa sheria wenye kuwajibika kwa wananchi, usawa wa jinsia, utu na
heshima ya kibinadamu kwa kila raia wakiwemo wanawake na wanaume,
watoto wa kike na wa kiume.Aidha, Katiba iwe inayowezesha uwepo wa
misingi mikuu ya usawa kati ya wanaume na wanawake katika vipengele
mbalimbali vya Katiba.
Bila shaka twapaswa kujua kuwa Katiba
ni‘Sheria Mama’ inayolinda haki za raia wote wakiwemo wanawake, wanaume
na watoto nchini na kuainisha mfumo wa kuendesha nchi na wajibu wa
viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza. Hivyo,ni vema Sheria hii Mama
iwe imebeba masuala ama haki za makundi haya mbalimbali nchini kwa
kudumisha maendeleo yenye tija.
Usawa wa jinsia ni msingi muhimu
kwenye maendeleo ya nchi yeyote ikiwemo nchi yetu Tanzania, ambapo
tafiti mbalimbali za hapa nchini na kwingineko zinaonyesha kuwa kwenye
sekta ambazo zinatekeleza mipango yenye kulenga katika kukidhi mahitaji
ya wanawake na wanaume pamoja na kutambua michango yao mbalimbali
zimeleta tija zaidi kimaendeleo.
Ujenzi wa misingi ya usawa wa
jinsia kwenye Katiba Mpya ni muhimu kwa kuwa Tanzania ni nchi mojawapo
ya Afrika na Ulimwenguni ambayo imesaini Mikataba mingi ya Kimataifa na
Kikanda ya kutekeleza Katiba, sera, sheria na mipango iliyojengewa
kwenye misingi ya usawa wa jinsia nchini.
Mikataba hii
inajumuisha Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa aina zote za Ubaguzi dhidi
ya Wanawake (CEDAW), Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto, Mpango wa
Utekelezaji wa Mikakati ya Beijing, Protokali ya Makubaliano ya Haki za
Binadamu na Usawa wa Jinsia ya Umoja wa Afrikapamoja na mikataba mingine
kadha wa kadha.
Hivi karibuni, tumeona ama kusikia juu ya Semina
iliyofanywa Bungeni mjini Dodoma na Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania
(TWPG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Wanawake na Katiba wakijadili juu
ya umuhimu wa uwepo wa masuala ya jinsia katika Katiba Mpya na masuala
muhimu ya jinsia ya kuzingatiwa katika katiba, ambapo wabunge hao
waliweka mkazo katika suala zima la haki sawa katika Katiba kati ya
wanawake na wanaume yani Hamsini kwa Hamsini.
Wabunge wanawake wa
Tanzania wakishirikiana kwa pamoja na Mtandao wa Wanawake na Katiba
waliweka bayana madai ya haki zao katika Katiba Mpyana madai haya ni
kama ifuatavyo;-
Haki za wanawake zibainishwe kwenye Katiba Mpya,
Sheria kandamizi zibatilishwe, Haki ya kufikia, kutumia, kunufaika na
umiliki rasilimali ya nchi,
Utu wa mwanamke ulindwe, Utekelezwaji
wa Mikataba ya Kimataifa kuhusu haki za wanawake, Haki sawa katika
nafasi za uongozi, Haki za Wanawake wenye ulemavu, Haki ya uzazi salama,
Haki za watoto wa kike, Haki ya kufikia na kufaidi huduma za msingi,
Wajibu wa wazazi katika matunzo ya watoto pamoja na Katiba iunde chombo
maalum kitakachosimamia haki za wanawake katika maeneo yote ya kijamii,
kisiasa na kiuchumi.
Kimsingi, madai haya yote ya haki sawa
yanayodaiwa na Wabunge hawa yana umuhimu mkubwa katika Katiba Mpya
itakayopatikana kwani ndiyo yatayopelekea kupatikana kwa Katiba yenye
mrengo wa jinsia.
Akitoa mada wakati wa semina hiyo, Mjumbe wa
Mtandao wa Wanawake na Katiba Bi. Usu Mallya alisema kuwa suala la
msingi wa usawa wa jinsia ni muhimu kuwekwa katika Katiba Mpya na
baadaye kuwepo na uwajibikaji wake kwani kwa kufanya hivyo kutaipatia
nchi katiba yenye mrengo wa kijinsia.
Bi. Mallya aliongeza kuwa
wanawake wengi nchini wamekuwa hawapati fursa ya usawa wajinsia katika
nyanja mbalimbali licha ya Tanzania kuwa kinara wa kutoa wanawake vinara
ambao wamewahi kushika nyazifa mbalimbali na wengine bado wakiendelea
kushika nafasi hizo za juu hapa nchini.
“Utafiti unaonyesha kuwa,
asilimia 5% ya wanawake nchini ndiyo wanaomiliki ardhi, asilimia 39% ya
wanawake hao hao hawapati elimu ya kutosha, pia utafiti unaonyesha kuwa
asilimia 40.3% ya wanawake walioko kwenye ajira wapo katika sekta isiyo
rasmi, wakati asilimia 10% ya Maprofesa wanawake ndiyo tunayo hapa
nchini”, alisema Bi. Mallya.
Aidha, Bi. Mallya alizitaja
changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake wengi nchini kuhusiana na
usawa wa jinsia na haki zao pamoja na haki za watoto huku akitoa taarifa
za utafiti zinazoonyesha kuwa mzigo wa kazi wa asilimia 66% ya wanawake
wanafanya kazi zisizo na kipato, na asilimia 44% ya wanawake nchini
walioolewa katika ndoa zao wamefanyiwa ukatili wa kijinsia.
Naye
Mwenyekiti wa Women Fund Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Mtandao wa
Wanawake na Katiba, Profesa Ruth Meena alizungumzia juu ya masuala ya
umuhimu wa jinsia ya kuzingatiwa katika Katiba Mpya huku akisisitiza juu
ya usawa wa uongozi katika ngazi zote uwe hamsini kwa hamsini na uwepo
wa chombo maalum kitakachozingatia haki za wanawake.
Profesa
Meena alisisitiza kuwa kuna umuhimu wa Katiba Mpya iweze kulinda haki za
watoto kwa kutoruhusu ndoa za utotoni, hivyo kuwepo na sheria zitakazo
mlinda mtoto dhidi ya ndoa hizo mpaka mtoto anapotimiza umri wa miaka
(18) Kumi na nane.
“Suala la umri wa mtoto wa kike kuolewa iwe ni
miaka Kumi na nane, na mtu atakayeoa mtoto chini ya miaka kumi na nane
awe amebaka”,alishauri Profesa Meena.
Aidha, Profesa Meena
aligusia kuhusu masuala ya haki ya uzazi salama kwa wanawake pindi
wanapojifungua, liweze kupewa kipaumbele kwa kujali usalama wa maisha ya
mama na mtoto na isiwe hukumu ya kifo kwa akina mama.
“Iwe ni
haki yetu ya uhai tunapofanya kazi ya kuongeza kizazi cha Tanzania,
wanawake wapewe usalama wa uzazi wanapozaa pasipokuwa na kigugumizi,
hivyo kuzaa kusiwe hukumu ya kifo kwa watoto wetu”,alisema Profesa
Meena.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la
Katiba, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye pia alihudhuria katika semina
hiyo, aliwatia moyo Wabunge wanawake hao na kuwataka kuwa na umoja wa
kudai haki zao za usawa wa jinsia na alisisitiza juu uwepo wa
ushirikiano kati ya wanaume na wanawake katika jamii.
Mhe. Samia
hapa anawataka wanaume kuwaunga mkono wanawake kwa kuwapa nafasi za
uongozi na waepuke tabia ya kuwadharau wanawake katika masuala
mbalimbali yakiwemo uongozi ama kuwapa talaka kutokana kuwa na hofu,
pindi wanawake wapatapo fursa ya uongozi.
Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba naye ameitaka jamii kuwekea
mkazo suala la elimu ya uzazi, kuwa ianze kutolewa kuanzia elimu ya
msingi ili watoto waweze kuwa na uelewa wa kutosha pindi wanapokuwa
wakubwa, Aidha alitoa hamsini kwa hamsini katika masuala yote katika
jamii.
Kwaupande wawajumbe wengine wa Bunge hilo, Mhe. Hamad
Rashid aliwashauri wanawake kuacha kutegemea Viti Maalum kwenye nafasi
za ubunge kwa kuwa kufanya hivyo kutasaidia kujenga uwezo na kujiamini
kuwa wanaweza.
“Mnapopata nafasi za uongozi mzitumie vizuri ili
kuweza kujiamini na kujituma,” alisisitiza Mhe. Hamad. NayeWaziri
Rajabu Salum mjumbe wa Bunge hilo, alisisitiza juu ya umuhimu wa elimu
kuhusu masuala ya kijinsia yatolewe kwa msuguano, kwani wanaume wengi
hawana uelewa wa jambo
hilo.
Agatha Senyagwa ambaye ni Mjumbe
wa Bunge hilo, kutoka kundi la 201 upande wa wakulima, alisema ni
vema elimu juu ya masuala ya kijinsia kwa wanawake wa vijijini ili
nao wawe na uelewa kwa ajili ya kushiriki katika kugombea nafasihususan
ngazi ya Serikali za Mitaa, mfano uwenyekiti wa kijiji na watendaji
kata.
Ili kufanikisha uwepo wa Katiba hii yenye mrengo wa jinsia,
hatunabudi kuingiza haki mahsusi (Gender specific) za wanawake na
watoto wa kike katika Katiba, pia kuingiza misingi imara ya usawa wa
jinsia na ile inayolinda haki za wanawake (Gender equality outcomes)
katika vipengele mbalimbali vya Katiba.
(Picha zote na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma).